Wakati Simba SC ikiwasili salama mjini Lilongwe nchini Malawi leo Alhamis (Septemba 08) tayari kwa mchezo wa Ligi ya Mabingwa Barani Afrika, Wawakilishi wa Zanzibar kwenye michuano ya Kombe la Shirikisho Afrika, Kipanga FC watawasili baadae Dar es salaam kutokea Unguja, kwa ajili ya mchezo wa Mkondo wa kwanza hatua ya awali dhidi ya Hilal FC Wau ya Sudan ya Kusini.

Kipanga FC itacheza mchezo huo ikiwa ugenini Uwanja wa Azam Complex, Dar es Salaam Jumapili (Septemba 12) majira ya saa 10 alasiri.

Hilal FC Wau imeomba kuutumia Uwanja wa Azam Complex kama wao wa nyumbani kutokana na hali ya machafuko nchini kwao, Sudan Kusini.

Kipanga itawasili Dar es salaam na msafara wa watu 30 wakiwamo wachezaji pamoja na viongozi wa timu hiyo.

Kocha Msaidizi wa timu hiyo, Khamis Hassan, amesema timu yake imejiandaa vizuri kuhakikisha inapata matokeo mazuri katika mchezo huo wa ugenini.

Amesema anajua mchezo wa ugenini utakuwa mgumu kwao, lakini wamejiandaa kuhakikisha wanasonga mbele katika michuano hiyo.

“Wachezaji wetu mpaka sasa wapo vizuri wote ambao tumewasajili kwa ajili ya michuano ya kimataifa wapo vizuri na wanaendelea na maandalizi ya mwisho mwisho kuelekea mchezo huo muhimu,”amesema.

Kipanga ipo chini ya Jeshi la Wananchi Tanzania (JWTZ) ambapo mchezo wao wa nyumbani utapigwa Uwanja wa Amaan, Zanzibar Septemba 16, mwaka huu.

Watoto Mil 1.3 wapata chanjo ya Polio
Muswada taarifa binafsi kuwafikia Wabunge