Licha ya mwaka 2021 kutegemewa utakuwa mwaka bora wa utoaji chanjo kwa watoto wachanga baada ya janga la Uviko-19 kuvuruga utoaji chanjo mwaka 2019 na 2020, ripoti iliyotolewa leo na Umoja wa Mataifa imesema kiwango cha utoaji chanjo duniani kimeendelea kupungua na kurudisha takwimu nyuma kwa miongo mitatu huku watoto milioni 25 wakikosa chanjo muhimu za kuokoa maisha yao.

Ripoti ya Pamoja, iliyotolewa leo jijini New York nchini Marekani na Geneva, Uswisi na mashirika mawili ya Umoja wa Mataifa ya Afya duniani WHO na la kuhudumia Watoto UNICEF imeeleza utoaji wa chanjo dhidi ya dondakoo, pepopunda, kifaduro ulishuka kwa asilimia tano mwaka 2019 na mwaka 2021 imeshuka hadi asilimia 81.

Ripoti hiyo, imefafanua kuwa kadri ripoti zinavyotoka kila mwaka zinaonesha jinsi watoto walivyo hatarini zaidi madhalani Watoto walikosa dozi moja au mbili za kujikinga kifaduro mwaka 2021 kupitia huduma za kawaidi walikuwa milioni 25, idadi hiyo ni milioni mbili zaidi ikilinganishwa na waliokosa chanjo hiyo mwaka 2020 na ni milioni 6 zaidi kwa Watoto waliokosa mwaka 2019.

Mtoto akipata matone ya chanjo.

Mkurugenzi Mkuu wa UNICEF, Catherine Russell ameonya kuwa ripoti hiyo ni hatari kwa afya ya Watoto na kwamba hata hivyo amesema hatari hiyo kubwa inaweza kuzuilika.

“Janga la covid-19 sio sababu tena ya kutotoa chanjo na bado tunashuhudia utoaji chanjo ukishuka. Tunapaswa kuhakikisha kuna upatikanaji wa chanjo kwa mamilioni ya watoto waliokosa chanjo hizo la sivyo tutashuhudia mlipuko zaidi wa magonjwa, watoto wengi wata ugua na hii itaongeza shinikizo kubwa katika mifumo ya afya ambayo kwasasa tayari ipo kwenye matatizo,” amesema.

Miongoni mwa sababu, zilizoelezwa kuchangia ongezeko la watoto kutopata chanjo ni pamoja na kuongezeka kwa watoto wanaoishi kwenye maeneo yenye mapigano au mazingira hatarishi kiusalama ambayo ufikishaji wa chanjo imekuwa changamoto, kuongezeka kwa taarifa za uongo na upotoshaji kuhusu chanjo pamoja na changamoto nyingine zilizosababishwa na janga la COVID-19 kama vile ugavi, usambazaji na hata huduma za utoaji chanjo kwa ujumla kukosekana.

Zoezi la utoaji chanjo

Mkurugenzi Mkuu wa WHO, Dkt. Tedros Adhanom Ghebreyesus amesema nchi zinapaswa kuhakikisha kila sekta ya afya inaguswa na sio kuachwa ili washuhulikie ugonjwa mmoja pekee na kudai kuwa mapambano ya Uviko-19 yanapaswa kwenda sambamba na mipango ya utoaji chanjo ya magonjwa kama surau, nimonia na kuhara.

Nchi zilizoathirika zaidi na ni zile za kipato cha chini na cha kati, ambapo nchi za India, Nigeria, Indonesia, Ethiopia na Ufilipino zinaongoza kwa kurekodi idadi kubwa zaidi ya watoto ambao hawajapata chanjo. Nchi nyingine ambazo mwaka 2021 watoto wengi walikosa chanjo ni Myanmar na Msumbiji.

Licha ya kushuka huko kwa utoaji chanjo duniani, lakini baadhi ya nchi ziliimarisha utoaji chanjo wake na kuzuia kushuka kwa takwimu na zimepongezwa kwa mikakati madhubuti pamoja na ushirikiano baina ya serikali na sekta ya afya.

Usimamizi sera kusaidia uzalishaji mbegu bora
Milioni 662 kukamilisha kituo cha afya Mtoa