Uongozi wa Klabu ya Mbeya City umepanga kuivurugia Sherehe za Ubingwa Young Africans, kwa kuhakikisha wanapata alama tatu muhimu katika mchezo wa Mzunguuko wa 29 wa Ligi Kuu Tanzania Bara.

Young Africans imeshatwaa taji la Ligi Kuu likiwa la 29 tangu 1965 baada ya kuifunga Dodoma Jiji FC kwa mabao 4-2 mwishoni mwa juma lililopita ikifikisha alama 74 huku ikiwa na michezo miwili mkononi itakayochezwa jijini Mbeya.

Mchezo wa kwanza utakuwa ni dhidi ya Mbeya City uliopangwa kupigwa Mei 24, kisha utafuata mchezo wa kufunga msimu dhidi ya Tanzania Prisons katika Uwanja wa Kumbukumbu ya Sokoine jijini Mbeya.

Uongozi wa Mbeya umesema hautakubali kuona timu yao inafanya vibaya katika mchezo huo, hivyo wamejipanga kuhakikisha Young Africans inaacha alama tatu, ambazo zitakuwa msaada mkubwa kwao.

Mmoja wa viongozi wa klabu hiyo ambaye hakutaka jina lake kuanikwa hadharani amesema, wanatambua baadhi ya Mashabiki na Wanachama wa Young Africans jijini Mbeya wanaendelea na vikao vyao kuhakikisha timu ya Mbeya City inapoteza mchezo huo, lakini amesisitiza hilo halitatokea.

Amesema wachezaji wana ari na morali baada ya ushindi dhidi ya Geita Gold, lakini hata sapoti wanayo pata kutoka kwa wadau na mashabiki va timu hiyo, inaendelea kuufanya Uongozi kuzidisha juhudi za kuhakikisha alama tatu zinapatikana.

“Ushindani ni mkali lakini kila mmoja ni kushinda mechi zake. Hatuangalii wa nyuma yetu wala wa mbele isipokuwa tunapambana na mechi zetu zilizobaki,” amesema kiongozi huyo

Ufukuaji wa miili: Wenyeji wavisaidia vyombo vya usalama
Mabalozi washiriki uletaji Watalii nchini - Mchengerwa